Kwa hakika ujasiriamali ni chaguo muhimu sana kwenye karne hii ya sasa
ili kujipatia kipato. Hivi leo kuna wajasiriamali wengi waliofanikiwa
na wengine hawajafanikiwa.
Kwa hakika wajasiriamali waliofanikiwa
wanafahamu na wanaziishi sifa za wajasiriamali bora. Ni wazi kuwa huwezi
kuwa mjasiriamali bora wakati una sifa za mwajiriwa.
Ili kuwa mjasiriamali ni lazima kuzifahamu na kuziishi sifa za mjasiriamali. Karibu nikufahamishe sifa 10 za mjasiriamali.
1. Mwenye malengo
Malengo
ni mwongozo wa kukuwezesha kufanikisha jambo lolote. Kuwa na malengo ni
sifa muhimu ambayo kila mjasiriamali anapaswa kuwa nayo. Je umeamua
kuwa mjasiriamali kwenye nini? Kwa ajili ya nini?
Malengo
yatakuongoza ufanye nini, wapi lini na kwa ajili ya nini. Bila malengo
utafanya mambo bila mwongozo wowote na ni vigumu kufanikiwa.
2. Nidhamu
Nidhamu
ni sifa muhimu kwa mjasiriamali kwani itamtenga na mambo mengi
yasiyokuwa na umuhimu. Ni lazima mjasiriamali awe na nidhamu ya maswala
kama vile matumizi ya muda pamoja na pesa.
Kila mjasiriamali anapaswa kujinyima na kukataa vitu vyote ambavyo havimwezeshi kufikia malengo yake.
3. Ujasiri na uthubutu
Ujasiri
na uthubutu ni sifa muhimu sana kwa mjasirimali ili aweze kutekeleza
malengo yake. Ujasiriamali ni swala linalohitaji ujasiri na uthubutu wa
kuchukua maamuzi magumu hata kama kuna changamoto au hatari kadha wa
kadha.
Huwezi kuwekeza pesa zako kwenye mradi au biashara yoyote
kama hutokuwa na ujasiri na uthubutu. Ujasiri na uthubutu hautaruhusu
hofu na mashaka ya kushindwa au kupata hasara vikutawale.
4. Ubunifu
Ubunifu
humtofautisha mjasiriamali mmoja na mwingine. Unahitaji ubunifu ili
ubuni wazo la pekee ambalo litakupa matokeo mazuri. Wajasiriamali wengi
hawana ubunifu ndiyo maana wanakwama.
Kwa mfano mjasiriamali mmoja
akianzisha biashara ya kuuza maandazi, basi wengine 20 wataiga. Ni
lazima mjasiriamali uwe na ubunifu utakaokuwezesha kufanya mambo yenye
tija.
5. Uvumilivu
Kila jambo lina changamoto zake. Ujasiriamali una changamoto nyingi ambazo zinahitaji uvumilivu ili kuzimudu.
Hivyo
basi, sifa ya kuwa na uvumilivu ni muhimu sana kwa kila mjasiriamali
anayetaka kufanikiwa. Haijalishi umepata hasara au unakutana na
changamoto nyingi kiasi gani, ni muhimu kuvumilia.
6. Bidii
“Mafanikio huja kwa wale ambao wanafanya bidii kubwa kuyatafuta.”
Bidii
ni msingi wa kufanikiwa kwenye jambo au shughuli yoyote. Ni muhimu
kukumbuka kuwa mjasiriamali ni mwajiri (boss) wake yeye mwenyewe. Hivyo
ni muhimu kujituma na kufanya kazi kwa bidii bila kusukumwa na mtu
yeyote.
7. Kupenda anachokifanya
“Fanya unachokipenda na pesa zitafuata.”
Watu
waliofanikiwa sana duniani, wanafanya kile wanachokipenda. Unapofanya
kile unachokipenda ni rahisi kufanikiwa kwani utakifanya kwa moyo, bidii
pamoja na kutokata tamaa.
Kila mjasiriamali anatakiwa kuhakikisha kuwa anafanya kitu anachokipenda ili aweze kufikia malengo yake.
8. Kuishi na watu vizuri
Kila
mjasiriamali anahitaji watu wengine ili kufanikisha malengo yake ya
ujasiriamali. Kuishi na watu vizuri ni sifa muhimu kwa mjasiriamali
kwani itamjengea soko zuri pamoja na nguvu kazi bora.
Hakuna haja
ya kudharau au kutenga watu bila sababu. Usijenge chuki au ugomvi
usiokuwa na sababu kati yako na watu wengine. Kumbuka kuwa watu ndio
chanzo na msingi wako wa kupata faida.
9. Mwenye kupenda kujifunza na mtafiti
Katika
swala zima la ujasiriamali, kutafiti na kupenda kujifunza ni tabia
muhimu sana. Kila mjasiriamali anatakiwa kuwa na sifa hii ili aweze
kujifunza na kutafiti njia na mbinu mbalimbali ambazo zinaweza kumfanya
mwenye tija zaidi.
Ni muhimu kukumbuka kuwa kuna wakati
mjasiriamali anatakiwa kukaa chini kutafiti na kujifunza mambo
mbalimbali ambayo yatamwezesha kufanikiwa kwenye kile anachokifanya.
10. Kujifunza kutokana na makosa
Kama ulivyowahi kusikia mara kadhaa kuwa makosa ni shule muhimu kwa kila mtu, ndivyo ilivyo pia kwa mjasiriamali.
Mjasiriamali
anapaswa kuwa na sifa ya kupenda kujifunza kutokana na makosa ili
asiyarudie tena mbeleni na wala si kuyaogopa au kuyakimbia.
Kama
uliwekeza pesa zako zikapotea, basi usiache ujasiriamali bali baini ni
nini kilisababisha ukapoteza pesa zako ili ukiepuke mbeleni.
Neno la mwisho
Naamini
ukiwachunguza vyema wajasiriamali waliofanikiwa utabaini kuwa wana
tabia hizi zilizoelezwa hapa. Ni muhimu wewe kama mjasiriamali
kuhakikisha unajitahidi kuwa na tabia zilizoelezwa hapa ili ufikie
malengo yako.
Je wewe una tabia hizi? Je umejifunza kitu kwenye makala hii?
Tafadhali
tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii.
Unaweza kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.
0 comments:
Post a Comment