Watu wengi wamekuwa wakitamani kuanza biashara lakini wanafikiri namna ya kuanza kwani mtaji wao ni mdogo sana.
Usiogope; kuwa na mtaji mdogo au kutokuwa nao kabisa sio mwisho wako wa kutimiza malengo yako.
“Usilie juu ya kile ambacho huna; tumia vizuri kile ulichonacho.”
Zipo
mbinu mbalimbali ambazo zinaweza kukuwezesha kufanya biashara hata kama
utakuwa na mtaji mdogo. Tafadhali fuatilia hoja jadiliwa hapo chini kwa
ufafanuzi zaidi.
1. Kuwa mbunifu
Moja kati ya mambo
ambayo yatakusaidia sana kwenye kuanza biashara kwa mtaji mdogo ni
ubunifu. Kwa njia ya ubunifu utaweza kushinda biashara na bidhaa
zilizoko sokoni kwa urahisi zaidi. Unaweza kufanya haya yafuatayo:
- Chagua wazo la biashara unalolipenda na kuliweza vyema. Hili litakusaidia kukabili changamoto vyema.
- Angalia tatizo au uhitaji uliopo sasa na uutatue kwa bidhaa au huduma yako.
- Panga bei vizuri; unaweza kuweka bei ambayo ni tofauti kidogo na bidhaa au huduma ambazo tayari ziko sokoni ili uwavutie wateja.
Kwa kufanya mambo yaliyoelezwa hapa juu utaweza kukuza biashara na mtaji wako kwa muda mfupi zaidi.
2. Anza na unachokijua
Unapokuwa
na mtaji mdogo huhitaji kuhusisha mambo mengi mageni au yanayotegemea
sana watu wengine kwa kuwa huna pesa za kuyagaramia.
Kwa mfano
kama unaanzisha biashara ya ushonaji basi anza kutengeneza mavazi yale
unayoyaweza kwa kutumia vifaa ulivyonavyo; kwa njia hii utajenga mtaji
wako kisha baadaye utaweza kuajiri wengine watakao kuwezesha kutengeneza
aina nyingine zaidi.
Unapofanya kile unachokijua gharama huwa haziwi kubwa sana kwani ni kitu unachokimudu mwenyewe.
3. Waambie watu unachokifanya
Waambie
watu unachokifanya kwani hili litakuwezesha kupata wateja na
kufahamika. Watu wakijua unachokifanya watatamani kukifahamu zaidi; hili
litakuwezesha kupata wateja na kuongeza mtaji wako.
Usiogope
kueleza kuwa unafanya biashara ya mboga, chakula, duka dogo la bidhaa
n.k. Kwani hujui unaemweleza atakuwa nani kwenye biashara yako.
Ukiwa na marafiki kwenye mitandao ya kijamii waeleze pia juu ya kile unachokifanya.
4. Epuka gharama zisizokuwa za lazima
Kwakuwa
bado una mtaji mdogo jitahidi kuepuka garama zisizo za lazima kama vile
ofisi ya kifahari, matangazo ya gharama kubwa n.k.
Kuwa na
matumizi mazuri ya fedha hasa kwa mambo ya msingi tu. Watu wengi
wameshindwa kwenye biashara kwa sababu wameanza biashara kwa mbwembwe za
matumizi badala ya huduma bora zenye ubunifu.
5. Fanya kazi kwa bidii
Kamwe
huwezi kuona mafaniko kama hutofanya bidii. Kumbuka wewe ni
mjasiriamali anayeanza hivyo ni lazima ufanye bidii ili soko litambue
kuwa upo pia unaweza.
Tumia muda vizuri,
pia hakikisha unatoa huduma yenye ubora wa hali ya juu kwa bei ambayo
wateja wataweza kuimudu. Jitese kwa muda mfupi kwa kipindi cha kuweka
msingi wa biashara yako kwani hata kipindi cha kupanda katika kilimo
huwa ni cha taabu.
6. Tumia rasilimali na fursa zilizopo
Njia
nyingine itakayokuwezesha kuanza biashara ukiwa na mtaji mdogo ni
kutumia fursa zilizopo. Kumbuka kuwa huwezi kutengeneza fursa kama
huwezi kutumia fursa zilizopo.
Tumia fursa kama vile mitandao ya
kijamii ili kujitangaza. Pia unaweza kutumia udhaifu uliopo katika
biashara nyingine za watangulizi wako kama fursa kwani unaweza
ukarekebisha udhaifu huo kupitia biashara yako.
Zipo pia fursa za
mikopo yenye masharti nafuu ambayo itakuwezesha kuongeza mtaji wako.
Kumbuka unahitaji kutumia mkopo kwa makini kwani utahitajika kuurudisha
pamoja na riba tena kwa wakati.
7. Jali wateja
Kujali
wateja katika biashara ni jambo muhimu sana kama unataka kuona matokeo
chanya. Siku zote ninapenda kusema “wateja hufugwa”. Wateja hufugwaje?
Hufugwa kwa huduma nzuri.
Waheshimu wateja wako pia hakikisha
unatimiza na kumaliza haja zao katika ubora wa hali ya juu. Kumbuka siku
zote mteja huja kwanza kabla ya pesa; hivyo usitangulize pesa kabla ya
huduma nzuri kwa mteja.
Ukilifanyia kazi hili utaweza kukuza biashara na mtaji wako kwa muda mfupi.
Hitimisho
Zilizojadiliwa
hapa ni mbinu saba zitakazokuwezesha kuanza biashara na mtaji mdogo.
Usiogope unaweza hata kama una kiasi kidogo sana cha fedha.
Thubutu, nza, fanya bidii, weka nidhamu, mtangulize Mungu na hakika utaona mafanikio chanya katika biashara yako.
“Anzia ulipo.Tumia ulicho nacho. Fanya unachoweza.”
Bado
umekwama katika eneo la kuwa na mtaji mdogo? Tafadhali tupe maoni yako;
pia karibu uwashirikishe wengine makala hii. Usisahau pia kufuatilia
ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.
0 comments:
Post a Comment